TANTRADE YASHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA MAONESHO YA CHAKULA NA KILIMO- AFRIKA (AFRO WORLD AGRI FOOD CONFERENCE AND EXHIBITION)






Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Taasisi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) tarehe 10 Agosti hadi 12 Agosti 2023,imeshiriki katika Maonesho ya  kilimo na chakula  Afrika (Afro World Agri Food Conference, exhibition) lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Upanga Dar es salaam,lenye lengo la kuwakutanisha wadau wa Chakula Afrika.


TanTrade ikiwa inatimiza moja kati ya majukumu yake ya kudhibiti Maonesho yote yanayofanyika nchini  ikiwa ni pamoja na Kusimamia  Viwango vya Maonesho ya  Kimataifa yanayofanyika Tanzania hivyo imefanikiwa kuhudhulia kikamilifu katika Maonesho hayo  ili kuhakikisha kuwa yanafuata sheria na Viwango vinavyotakiwa katika kuendesha Maonesho.


Sambamba na  dhima mbalimbali katika Maonesho haya, pia Maonesho yalienda sambamba na Mikutano ya ana kwa ana kwa Wafanyabiashara (B2B) iliyowakutanisha Wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta ya Chakula, Viungo, Korosho, Sukari,Maharage , Ngano Pamba, kahawa,  pamoja na Kakao.

Akizungumza katika maonesho  hayo Afisa Biashara kutoka TanTrade Bw.Melkizedeck Salingo amesema kuwa, maonesho hayo   yamekuwa  muhimu sana kwa wadau wote wa Biashara katika Sekta ya Chakula kwani yamewezesha Wadau kujuana kwa ukaribu chini ya Mwamvuli wa Biashara  na kubadilishana mawazo na wadau wengine na kujipatia masoko ya bidhaa zao. 

Aidha  Bw. Salingo ametembelea katika Mabanda mbalimbali ya Wafanyabiashara kutoka India na kuwaelezea majukumu ya TanTrade pamoja na kuwatia  moyo wawekezaji hao kuja kuwekeza na kufanya biashara na nchi ya Tanzania, kwani Tanzania ni mahali sahihi kwa kufanya biashara pamoja na Uwekezaji. 

Naye mmoja kati ya waandaji wa maonesho hayo Bw. Suveer Raj Proheit  ametoa wito kwa wadau wote wa Chakula na Kilimo, kuendelea kujitokeza na kuunga mkono maonesho hayo ili kujihakikishia Masoko ya bidhaa wanazozalisha.

‘’Nawashukuru Wadau wote walioshiriki katika maonesho haya, Hakika wamepata faida kubwa ya kuwepo mahali hapa ikiwemo kujipatia Masoko ya bidhaa wanazozalisha na sambamba na kupata wadau mbalimbali wa kufanya nao kazi, pia napenda Kuchukua fursa hii  kuwakaribisha Wadau wengi zaidi wajitokeze katika  maonesho kwa mwaka ujao’’. Alisema.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TanTrade

 

KAMATI YAIPONGEZA TANTRADE KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TanTrade kwa kuboresha mazingira ya biashara hususani Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2023.

Vilevile Kamati hiyo imeiagiza TanTrade kupitia Sheria na kuwa na mikakati mahususi  ikiwemo ya uboreshaji wa miundombinu  katika maonesho ya sabasaba na utafutaji wa masoko kwa bidhaa za Tanzania inayoendana na wakati na mabadiliko ya Teknolojia

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti  wa Kamati hiyo Mhe. Mariam Ditopile (Mb.) Agosti 15, 2023 wakati ikipokea Taarifa ya Hali Halisi ya Utendaji wa Majukumu ya TanTrade katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Aidha, wajumbe hao walipata fursa ya kutoa  maoni mbalimbali kuhusu uendelezaji wa biashara hususan mauzo ya nje, utafutaji wa masoko, biashara mtandao na mapendekezo ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ukuzaji wa  biashara  

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe(Mb.) akijumuisha maoni na mapendekezo hayo ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo yatatekelezwa  ili kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara, kukuza biashara na mauzo ya ndani na nje   na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara aliieleza Kamati hiyo kuwa Wizara imeanza kupitia na kurekebisha Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria inayosimamia TanTrade ili ziendane na wakati na mabadiliko ya teknolojia

Awali Mkurugenzi  Mkuu wa TanTrade Bi Latifa Mohamed  akiwasilisha taarifa ya Taasisi yake kwa Kamati hiyo, amesema jukumu kuu la TanTrade ni kukuza na  kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi ili kuimarisha biashara yenye tija katika maendeleo ya kiuchumi nchini.