6TH CIIE -SHANGAHAI CHINA

 

Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano, TANTRADE wakutana na East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC)- Shanghai


Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Nyumba Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji wawakilishi wa TanTrade wakiongozwa na Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara Bw. Fortunatus Mhambe na mwakilishi  kutoka Kampuni ya Kahawa ya Africafe Bw. Abdulhakim Mulla walikutana katika ofisi kuu ya EACLC iliyopo Shanghai-China kwa ajili ya kusikiliza wasilisho kutoka kwa Lisa Wang  ambaye ni Mwenyekiti wa EACLC ambaye katika wasilisho lake alishukuru Serikali ya Tanzania kuendelea kuipa fursa ya kiuwekezaji kampuni yake ya EACLC.

Lisa alitumia wasaa huo kuorodhesha miradi ambayo kampuni yake  inaendelea na utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na
- Mradi Mkubwa wa Soko Kuu La Kimataifa la Afrika Mashariki -Ubungo Dar Es Salaam linaloendelea na ujenzi wake ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024 ambao utakuwa na maduka zaidi ya 2,000 na kufanya Jiji la Dar Es Salaam kupokea wageni kutoka takribani nchi 9 ambazo zitakuwa zikinunua bidhaa hapo badala ya kusafiri mpaka nchini China.

-  Mradi wa Ujenzi wa Hospitali Zanzibar na
- Mradi wa Maghala ya Uhifadhi wa Bidhaa  zitakazouzwa nje ya nchi na zitakazoletwa nchini Tanzania utaokuwa maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar

Vilevile Lisa Wang aliongeza kwa kuishukuru TanTrade kwa kuendelea kuiunga mkono kampuni ya  EACLC na kusema kuwa kutokana na ushiriki wao mzuri katika Maonesho ya Sabasaba {DITF} ya 47 ya 2023 wafanyabiasha wengi zaidi kutoka China wameonesha nia ya kushiriki katika Maonesho yajayo ya 48 ya DITF, 2024.

Aidha, Bi. Lisa Wang ameahidi kuendelea kuitangaza Tanzania ikiwamo kushiriki katika Maonesho yatakayofanyika Januari, 2024 Zanzibar.

Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China alimwakikishia Lisa Wang kuwa Serikali inatambua Mchango Mkubwa EACLC inafanya kwa nchi ya Tanzania na kuwa wataendelea kumpa ushirikiano.

Naye Bw. Fortunatus Mhambe ambaye ni Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara alimpongeza Lisa kwa kuleta washiriki wa Maonesho ya Sabasaba kutoka China wapatao 187. Aidha, alimpongeza Lisa kwa kampuni yake kudhamini Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar Es Salaam ya 2023

Ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Sita ya Bidhaa na Huduma (6th International Import Expo -CIIE ) ya Shanghai - China ambayo yameanza tarehe 5 hadi 10 Novemba, 2023


Maonesho hayo ambayo yanatoa fursa kwa nchi mbalimbali kuuza bidhaa nchini China yalifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa China  Mheshimiwa Li Qiang.

Katika Maonesho haya nchi zaidi ya 127 zinashiriki zenye zaidi ya Waoneshaji 2800. Aidhaa bidhaa mbalimbali za Kilimo, Mazao Teknolojia na Ubunifu mpya 438 zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 73.52 zinaoneshwa.

Katika Maonesho haya kutakuwa na mikutano 24 ya kibiashara na uwekezaji ambayo itahudhuriwa na Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi za Biashara na Uwekezaji na Sekta Binafsi wakikutanishwa na taasisi mbalimbali na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa wakiwemo ITC, WTO UNDP na UNIDO.

Aidha, katika mikutano hiyo fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji zitajadiliwa kwa undani.

Maonesho haya ya 6 ya Huduma na Bidhaa ya China (CIIE) ni fursa nzuri kwa wafanyabiashara watanzania kuonesha Bidhaa na Huduma zao kwa jamii ya China na kuweza kuwaunganisha na masoko ili kukuza mitaji yao na kukuza uchumi wa Taifa kiujumla.

Msafara wa washiriki kutoka Tanzania katika Maonesho haya waliongozwa na Maafisa kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) chini ya Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara, Bw. Fortunatus Mhambe. Washiriki katika Maonesho haya kutoka Tanzania ni pamoja na ZAFICO, PBZ, TRA, ZBS, Africafe na KMVL.

Aidha, TANTRADE imesimamia ushiriki wa baadhi ya makampuni na taasisi  ambazo zimewasilishwa sampo bila ushiriki wao binafsi ikiwamo kampuni Ya AMIMZA inayouza kahawa nje ya nchi.

WAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI YA TANTRADE WAPATA SEMINA YA UONGOZI

Tarehe 20 Oktoba, 2023.
DAR ES SALAAM

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) wamepata semina ya Uongozi iliyotolewa na Taasisi ya Uongozi Institute kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina kuanzia tarehe 19 - 20 Oktoba, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa TanTrade Jijini Dar es Salaam.

Semina hiyo ya siku mbili ilihusisha mada zikiwemo Uendeshaji wa Shirika na Uongozi Bora, Kufikia Ufanisi wa Bodi, Usimamizi wa Vihatarishi na Msingi wa Udhibiti wa Ndani pamoja na Usimamizi wa Fedha.

Akiongea katika Kufungua rasmi semina hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya TanTrade, Prof. Ulingeta Obadia Mbamba alieleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa wajumbe wa Bodi ambapo yanatarijiwa kuongeza Ufanisi zaidi kwenye Utendaji wa Bodi na kuongeza tija kwenye utekelezaji na Usimamizi wa majukumu waliyonayo kama Wajumbe  wa Bodi ya Wakurugenzi wa  Mamlaka. 

TANTRADE YAPATIWA UTAALAM WA KUENDELEZA BIASHARA MTANDAO NCHINI CHINA


Hangzhou, Zhejiang
China
3 Novemba 2023.

Kwa kutambua majukumu ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ambapo hutekelezwa  sambamba na utekelezaji wa
Ilani ya Chama Tawala, Chama cha Mapinduzi( CCM)  kilitoa fursa kwa TanTrade kupata mafunzo kwa ajili ya kozi ya E-commerce nchini China. Ufadhili huo ulikuwa chini ya Wizara ya Biashara ya China unaotokana na uhusiano mzuri uliopo katika nyanja mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.

Katika kozi hii, watendaji wanne, kutoka CCM (2), TanTrade(1) na DART(1) walioteuliwa  kupata mafunzo  mahususi kuhusu
Biashara ya mtandao (E-commerce) kuanzia Oktoba 13 hadi Novemba 3, 2023. Mafunzo haya yaliyofanyika katika mji mkuu wa Teknolojia wa Hangzhou, Jimbo la Zhejiang (wakazi milioni 160) yaliendeshwa na Bodi ya Maendeleo ya Biashara Huria ya Zhejiang(ZFTDB) kwa ufadhili wa Wizara ya Biashara - China.

Washiriki wengine muhimu waliotoka nchi zinazoendelea ni pamoja na Sierra Leone, Oman, Pakistan, Cameroon, Nigeria na Mongolia.

Utaalam huu unatolewa wakati biashara za mtandaoni zinaonekana kushika kasi duniani, hasa baada ya janga la COVID-19 ambapo wafanyabiashara wanatumia mifumo ya kisasa ya mtandao, akili bandia (AI) na mitandao ya kijamii katika kutafuta masoko, bidhaa na wateja na pia kuuza kwa njia za moja kwa moja ni kupitia Utiririshaji wa moja kwa moja wa video.

Wataalam wamepata maarifa mengi juu ya jinsi ya kuunganisha uchumi wa kidijitali, biashara ya mtandaoni na ukuaji wa miji na utalii, mbinu za masoko ya mtandao na bei, uundaji wa vituo vya biashara na miundombinu wezeshi, mauzo na manunuzi kwenye mtandao na kuona kwa wenyewe jinsi masoko ya miji muhimu ya Hangzhouh (teknolojia), Zhuji (vito), Putian (viatu) na Tongxian (mavazi) iliyoko Zhejiang China yanavyofanya kazi kwa ufanisi.
Vile vile, wataalam waliotembelea na kusikiliza mihadhara iliyotolewa na makampuni yanayoongoza katika biashara ya mtandaoni ya mpakani ikijumuisha Alibaba Group, Dahua Technologies, SunHigh na Wensli Silk na Chinagoods.com; ambapo biashara za mtandaoni huchangia zaidi ya asilimia 30 katika mapato ya Jiji la Zhejiang na kuchangia wastani wa yuan bilioni 279 kwa mwaka.

Wataalamu hao wameishukuru Serikali na vyama hivyo kwa kuendelea kukuza Diplomasia ya Uchumi na Biashara na kuahidi kutumia elimu waliyoipata kulitumikia Taifa katika kukuza Biashara na uchumi kwa kuendelea kuwajengea uwezo na ushauri kwa watendaji, Taasisi na wajasiriamali.
------------------------------------
Picha: Tuzo za vyeti kwa maafisa wanne wa Kitanzania na wahitimu wenzao.

TANTRADE YASHIRIKI MKUTANO WA MAANDALIZI YA EXPO 2023 DOHA


10 Septemba, 2023.

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeshiriki mkutano wa mwisho wa maandalizi ya Expo 2023 Doha unaofanyika tarehe 10-11 Septemba, 2023, Doha, Qatar.

Mkutano huo umeshirikisha Makamishna wakuu wa Nchi 56 Duniani zinazoshiriki Maonesho ya Kilimo cha Mboga Mboga yanayojulikana kama Doha Horticultural Expo ukiwa ni muendelezo wa matayarisho hayo ambapo Timu ya Expo iliwasilisha hatua za matayarisho kwa makamishna hao ili kurahisisha ushiriki wao katika maonesho yanayotarajiwa kuanza tarehe 2 Octoba, 2023 hadi 28 Machi 2024.
Kwa upande wa Tanzania, mkutano umewakilishwa na Bw.Tahir M.Ahmed na Bi. Mwanaidi K. Chilo kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Banda la Tanzania, Bi. Latifa M. Khamis, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade.

TANTRADE KUSHIRIKI KATIKA UFUNGUZI WA MAFUNZO YA UJASILIAMALI KWA WANAWAKE


DAR ES SALAAM.
12 SEPTEMBA, 2023

Mamlaka ya Maendeleo na Biashara Tanzania (TanTrade) kushiriki na wafanyabiashara katika  ufunguzi wa mafunzo na kufanya mdahalo kuhusu   Ujasiliamali katika ukumbi wa Kibada Garden Kigamboni- Dar es salaam tarehe 12 Septemba, 2023.

Ambapo, Afisa wa TanTrade Bi.Lulu Masanje amesema Mamlaka ya Maendeleo na Biashara Tanzania inatoa mafunzo juu ya kujikwamua kibiashara ndani na nje ya nchi ambapo jukumu la kwanza ni kutoa taarifa mbalimbali za biashara ambazo zinampa fursa mfanyabiashara kufahamu kuhusu takwimu ambazo  bidhaa zinauzwa sana na kuongeza soko kwa wingi zaidi na itamsaidia mfanyabiashara kufanya maamuzi sahihi kwaajili ya kujikwamua kiuchumi.

Vilevile, TanTrade inatoa fursa za masoko, mabanda ya maonyesho na usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi mbalimbali ambapo fursa hizi   zitachangia katika kuongeza uchumi binafsi na nchi kwa ujumla. Kadhalika, kutambua takwimu za bidhaa zinazouzwa na nchi mbalimbali kama vile korosho, kahawa, pamba na parachichi.

Pia, kuhusu suala la nishati, TanTrade imeweza kushirikiana na Kenya katika usambazaji wa nishati ya kisasa na iliyo salama na itaendelea kujumuisha nchi mbalimbali ilikukuza soko la nishati vilevile,katika mdahalo amewashauri wajasiliamali kuhusu ufanyaji wa utafiti kabla ya kuleta bidhaa sokoni kwani itasaidia katika kutambua mahitaji ya wateja na kupata njia mbalimbali za kuwa hudumia.

TANTRADE YAENDELEA KUTOA FURSA ZA “INTERNSHIP” KWA WANAFUNZI WA VYUO MBALIMBALI HAPA NCHINI.

 

Mikutano ya Usalama wa Chakula Africa(AGRF 2023).

 

TANTRADE YAWAJENGEA UWEZO WANAFUNZI WA MASOMO YA BIASHARA NCHINI ILI WAZIJUE SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA UFANYAJI BIASHARA ZILIZOWEKWA NA SERIKALI.


.................................
 TanTrade Dar es salaam.
 18 Agusti 2023.

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Leo Tarehe 18 Agusti 2023, imetoa Mafunzo  kwa Wanafunzi wa kidato cha tano wa shule ya Sekondari BaoBab iliyopo jijini Dar es salaam, yenye  malengo ya kujua kazi za TanTrade na kuwajengea uwezo Wanafunzi hao ili kuelewa ni kwa namna gani TanTrade  inafanya kazi ili kuwasaidia Jumuiya ya Wafanyabiashara, pamoja na kufahamu miongozo mbalimbali ya Ufanyajibiashara nchini.

 
Mafunzo hayo yamefanyika Leo Tarehe 18 Agusti 2023 katika ukumbi wa TanTrade uliopo barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.


Akitoa mada katika Mafunzo hayo Afisa Biashara kutoka TanTrade Bi. Marcelina Antony amesema TanTrade ni Taasisi ya Serikali iliyopewa Mamlaka ya udhibiti, utendaji,  na ushauri wa kuendeleza na kukuza biashara za ndani na nje ya Tanzania.
Hivyo Wafanyabiashara wengi wamenufaika kupitia TanTrade kwa kujengewa uwezo wa kuwezeshwa kufanya biashara kiutaalamu na kiushindani kupitia Mafunzo ya Biashara.

Pia TanTrade imefanikiwa kuwaunganisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na wauzaji na wanunuzi kutoka nje ya nchi, na kuwasaidia  Wafanyabiashara kukua kibiashara kupitia Maonesho ya biashara yanayoratibiwa na TanTrade kama vile , Maonesho ya SabaSaba pamoja  na misafara mbalimbali ya biashara.

Naye Afisa Biashara kutoka TanTrade Bi.  Mwanaidi Chiro ameongeza kuwa  TanTrade pia inahusika na  Wafanyabiashara wanaofuata sheria za nchi za Ufanyaji biashara  na inaandaa  Makongamano mbalimbali ya kibiashara, kwa mfano  kongamano la sudani  ambapo tulipata oda ya Mahindi na tulitangaza huduma zetu  za afya kama vile huduma zinazotolewa na hospitali ya  Muhimbili, Kwa kufanya hivyo  tulitangaza bidhaa na  huduma zinazozalishwa na Watanzania na kusaidia  Wafanyabiashara  kupata Masoko makubwa ya nje ya nchi. 

Sambamba na hayo TanTrade pia ina jukumu la kuratibu misafara na Makongamano mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania.


"Kama kuna Waoneshaji wanatoka nje ya nchi na  kuja Tanzania kuonesha bidhaa zao, wanakaguliwa kama wamekidhi vigezo na kufuata sheria za uoneshaji ikiwa ni pamoja na kuomba  vibali na kukamilisha  taratibu zote.  hivyo Serikali inahusika na  utengenezaji wa  Mazingira wezeshi ya kufanya biashara, ikiwa ni  pamoja na kutengeza mifumo wezeshi na rafiki ili kuhakikisha kwamba muuzaji anaweza kuuza na kununua biashara.’’ Alisema.



Aidha Afisa Biashara kutoka TanTrade Bw. Melchizedek Salingo aliongeza kuwa TanTrade inawasaidia Wafanyabiashara kwa   kufanya utafiti wa Soko la ndani na Soko la nje ili kujua ni bidhaa zipi zinazohitajika sokoni ili Wafanyabiashara waweze kuzalisha na kutoa huduma inayotokana na mahitaji ya Soko husika.

Naye Mwalimu wa somo la Biashara kutoka shule ya sekondari ya BaoBab Mwl. Mtinda kengela kwa niaba ya shule ya BaoBab ametoa shukrani kwa Uongozi wa TanTrade kwa kuwapokea na kuwapa mafunzo Wanafunzi hao  yatakayowajenga kibiashara.

TANTRADE YASHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA KIKAO KAZI CHA WENYEVITI WA BODI NA WATENDAJI WAKUU WA TAASIS ZA UMMA.


TANTRADE YASHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA KIKAO KAZI CHA WENYEVITI WA BODI NA WATENDAJI WAKUU WA TAASIS ZA UMMA.

Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (TanTrade) ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bi. Latifa Khamis imeshiriki katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kilichofanyika Agosti 19, 2023 Jijini Arusha.

Katika Kikao hicho cha Kazi
Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye amewasisitiza Watendaji Wakuu wa Taasisi hiyo kuweka Uzalendo mbele katika kutekeleza majukumu yao na kuwa sehemu ya mabadiliko chanya.
Pia amewataka kuwa tayari kwa mageuzi katika Taasisi za Umma kwa Maendeleo ya Taifa

Pia alieleza kuwa kutakuwa na ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini ili kufikia malengo na kuleta tija kwa Taasisi hiyo.

August 28, 2023

 

TANTRADE WAUNGANISHA KAMPUNI ZA TANZANIA NA KAMPUNI YA MAGNIT KUTOKA URUSI 30 AGOSTI 2023

 

28 AGOSTI 2023 DAR ES SALAAM

 

TANTRADE YASHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA MAONESHO YA CHAKULA NA KILIMO- AFRIKA (AFRO WORLD AGRI FOOD CONFERENCE AND EXHIBITION)






Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Taasisi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) tarehe 10 Agosti hadi 12 Agosti 2023,imeshiriki katika Maonesho ya  kilimo na chakula  Afrika (Afro World Agri Food Conference, exhibition) lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Upanga Dar es salaam,lenye lengo la kuwakutanisha wadau wa Chakula Afrika.


TanTrade ikiwa inatimiza moja kati ya majukumu yake ya kudhibiti Maonesho yote yanayofanyika nchini  ikiwa ni pamoja na Kusimamia  Viwango vya Maonesho ya  Kimataifa yanayofanyika Tanzania hivyo imefanikiwa kuhudhulia kikamilifu katika Maonesho hayo  ili kuhakikisha kuwa yanafuata sheria na Viwango vinavyotakiwa katika kuendesha Maonesho.


Sambamba na  dhima mbalimbali katika Maonesho haya, pia Maonesho yalienda sambamba na Mikutano ya ana kwa ana kwa Wafanyabiashara (B2B) iliyowakutanisha Wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta ya Chakula, Viungo, Korosho, Sukari,Maharage , Ngano Pamba, kahawa,  pamoja na Kakao.

Akizungumza katika maonesho  hayo Afisa Biashara kutoka TanTrade Bw.Melkizedeck Salingo amesema kuwa, maonesho hayo   yamekuwa  muhimu sana kwa wadau wote wa Biashara katika Sekta ya Chakula kwani yamewezesha Wadau kujuana kwa ukaribu chini ya Mwamvuli wa Biashara  na kubadilishana mawazo na wadau wengine na kujipatia masoko ya bidhaa zao. 

Aidha  Bw. Salingo ametembelea katika Mabanda mbalimbali ya Wafanyabiashara kutoka India na kuwaelezea majukumu ya TanTrade pamoja na kuwatia  moyo wawekezaji hao kuja kuwekeza na kufanya biashara na nchi ya Tanzania, kwani Tanzania ni mahali sahihi kwa kufanya biashara pamoja na Uwekezaji. 

Naye mmoja kati ya waandaji wa maonesho hayo Bw. Suveer Raj Proheit  ametoa wito kwa wadau wote wa Chakula na Kilimo, kuendelea kujitokeza na kuunga mkono maonesho hayo ili kujihakikishia Masoko ya bidhaa wanazozalisha.

‘’Nawashukuru Wadau wote walioshiriki katika maonesho haya, Hakika wamepata faida kubwa ya kuwepo mahali hapa ikiwemo kujipatia Masoko ya bidhaa wanazozalisha na sambamba na kupata wadau mbalimbali wa kufanya nao kazi, pia napenda Kuchukua fursa hii  kuwakaribisha Wadau wengi zaidi wajitokeze katika  maonesho kwa mwaka ujao’’. Alisema.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TanTrade

 

KAMATI YAIPONGEZA TANTRADE KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TanTrade kwa kuboresha mazingira ya biashara hususani Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2023.

Vilevile Kamati hiyo imeiagiza TanTrade kupitia Sheria na kuwa na mikakati mahususi  ikiwemo ya uboreshaji wa miundombinu  katika maonesho ya sabasaba na utafutaji wa masoko kwa bidhaa za Tanzania inayoendana na wakati na mabadiliko ya Teknolojia

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti  wa Kamati hiyo Mhe. Mariam Ditopile (Mb.) Agosti 15, 2023 wakati ikipokea Taarifa ya Hali Halisi ya Utendaji wa Majukumu ya TanTrade katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Aidha, wajumbe hao walipata fursa ya kutoa  maoni mbalimbali kuhusu uendelezaji wa biashara hususan mauzo ya nje, utafutaji wa masoko, biashara mtandao na mapendekezo ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ukuzaji wa  biashara  

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe(Mb.) akijumuisha maoni na mapendekezo hayo ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo yatatekelezwa  ili kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara, kukuza biashara na mauzo ya ndani na nje   na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara aliieleza Kamati hiyo kuwa Wizara imeanza kupitia na kurekebisha Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria inayosimamia TanTrade ili ziendane na wakati na mabadiliko ya teknolojia

Awali Mkurugenzi  Mkuu wa TanTrade Bi Latifa Mohamed  akiwasilisha taarifa ya Taasisi yake kwa Kamati hiyo, amesema jukumu kuu la TanTrade ni kukuza na  kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi ili kuimarisha biashara yenye tija katika maendeleo ya kiuchumi nchini.